Je, Waijua Thamani Ya UCHI wako?

Unaweza kuwa mmoja wapo wa watu ambao wametaharushwa na kichwa cha andiko hili. “UCHI” ni neno ambalo limevishwa maana na mtazamo potofu katika utandawazi wa usasa. Tafsiri yangu: “Uchi ni hali ya utupu, hali ya kuwa kamilifu bila kuhitaji ziada ya nje.”

Ni dhahiri kuwa kila mtu amezaliwa akiwa UCHI, yaani ana ukamilifu wa utu na uwezo wa kukamilisha safari yake na kusudi la kuletwa Duniani. Bila kufungashiwa mzigo wa kifaa ama kiambata cha kumuwezesha kukamilisha safari ya maisha. Kila kitu ulicho hitaji kuwa nacho katika ukamilifu wa thamani yako, ulizaliwa nacho ukiwa uchi. 

Hivyo basi, thamani yako iko kwenye uchi wako “Hali ya kutokuwa na kitu kingine nje ya wewe”

UCHI ni ukamilifu usio hitaji ziada, tunazaliwa tukiwa uchi na kamilifu, wenye tunu na thamani isiyopimika, na yanye utofauti na kiumbe mwingine awae yote. Na katika ukamilifu huo, ndimo kumejaa matunda ambayo baadhi yake yanadhihirika katika hali na mali. 

Ni watu wachache ambao wamefanikiwa kuyatofautisha mafanikio yao na hali yao ya uchi, wengi wanayatafsiri mafanikio kwa kigezo cha hali na mali.

Utakapo fanikiwa kutofautisha na kutenganisha maisha yako na mafanikio yako ya hali na mali. Utaishi maisha kamilifu na yenye kusudi. Na utakuwa mtu mwenye furaha ambayo itakuletea mafanikio.

Kumbuka mwenye ziada hatumii kumshinda asiye na ziada. Ukiwa na nguo kenda, muda wa kuvaa lazima utaivaa moja. Ukiwa na magari 100 ya farasi, wakati wa safari utatumia gari moja.
Mafanikio hayaleti furaha, bali furaha inaleta mafanikio. Unazaliwa ukiwa uchi na utakufa ukiwa uchi, thamani yako ipo katika hali yako ya uchi.

Itambue thamani yako ukiwa uchi

%d bloggers like this: