Je? Wewe ni Mbuzi Kati ya Kundi la Kondoo

Kitakuwa ni kitu cha kushangaza sana endapo mtu ataimbisha wimbo wa mbio za Mwenge kwenye shughuli ya msiba. Au mpishi kuweka sukari kwenye pishi la wali ati. Hii yote ni kwa sababu kila mazingira yana taratibu zake na zikikiukwa basi kunatokea mkanganyiko wa mfumo mzima wa tukio au jamii husika.
Kawaida ni kwamba binaadamu huwezi kuwa katika eneo zaidi ya moja kwa wakati mmoja, ndiyo uhalisia wa mambo. Na kila unapobadili eneo unavaa uhusika wa tabia za eneo hilo, na huu ndio utashi wa binaadamu unaotutofautisha na wanyama pamoja na viumbe wengine.
Ukiwa msibani, utakuwa na utulivu na kufuata taratibu za kuwepo majonzini, ukiwa uwanja wa soka basi utapiga bashasha na kushangilia ipasavyo, ukiingia nyumba ya ibada basi utavaa utulivu na unyenyekevu sawa sawa na mazingira ya ibada. Vivyo hivyo ukiongea na watoto utakuwa na maneno ambayo yataeleweka kwa watoto hao, na ukibadili nafasi na kuongea na watu wazima zaidi yako utatumia lugha ya staha na kuonyesha heshima kwao. Lakini utakapo kuwa na wenzako, watani wako basi utafanya utani sawia na mazingira ya watu unaotaniana nao. Ukifanya kinyume na haya, basi hali nzima ya uwepo wako inakuwa na mtazamo tofauti na wa taharuki, na kuonekana hufai kwenye eneo la hiyo jamii.
Katika mitandao ya kijamii, tumeona jinsi ambavyo inawezekana kuwepo maeneo mengi kwa wakati mmoja kwa kutumia nguvu ya simu ya mkononi “smart phone”. Una uwezo wa kuwasiliana na makundi kadhaa kwa wakati mmoja, yakijumuisha watu toka nchi mbalimbali na watu wa rika na staha tofauti. Mambo haya yote ni muhimu sana na yana tija pale yanapotumika sawasawa na makusudio yake. Lakini utaratibu unapokiukwa, yanageuka kuwa karaha na kuondoa kabisa ile maana halisi ya lengo la kuundwa kwake.
Mfano, chukulia mtu yupo kwenye kundi la WhatSapp ama Facebook la Alumni wa chuo fulani, watu hawa wanatoka katika maeneo tofauti, wana nyadhifa tofauti, wana imani tofauti nakadhalika. Hapa ni lazima kila mwanakundi atumie utashi wake kuelewa ni mambo ya aina gani yanafaa kuongelewa kwa kundi hili, heshima na staha ikiwa ni kitu cha msingi, na sio heshima kwa wanakundi tu, bali hata wewe kujiheshimisha kwao kwa michango yako na maoni yako. Michango yako ya mawazo, maoni, picha nk Je ina mchango gani jengefu kwenye jamii husika ya hilo kundi? Maana muda ni mali na gharama, hivyo kuchangia mambo yasiyo na tija, ni kupoteza muda wa watu wengine wengi, kambo ambalo sio heshima pia.
Mfano mwingine, inatokea mtu ameingia kwenye kundi lenye madhumuni ya kupeana ushauri nasaha kuhusu kilimo, yeye anashusha picha 100 za biashara yake ya vitenge. Ama kundi la kwaya ya waimbaji fulani wa kidini, halafu mtu anatuma vibonzo vyenye mlengo tofauti kabisa na lengo la kundi.
Mambo haya ni mfano mdogo sana wa jinsi gani watu wengi tunashindwa kufahamu mipaka na malengo halisi ya makundi tunayohusika nayo. Na kwa kufanya hivi, tunapoteza sana tija na umuhimu wa hizi njia za mawasiliano, na kufanya wengine kuona ni upuuzi tu kuhusika na mitandao.
Wenzetu wenye kuelewa mipaka hii, wamekuwa wakitumia makundi haya kujijenga, kusimamia kazi, kuzalisha na hata kupeana ushauri mahsusi katika mambo yao ya msingi na kujijenga kila siku. Makundi na njia hizi za mawasiliano zinatumika kujenga jamii bora, yenye kujitambua na kujikwamua katika maswala mbali mbali yanayohusu maendeleo ya jamii husika. Lakini yote haya yanatokana na uelewa wa mahali, mazingira na maudhui ya kundi na mawasiliano husika.
Mwisho nitoe rai kwa jamii yetu, hasa sisi wageni wa mitandao na teknolojia ya mawasiliano ya kisasa. Kufahamu jinsi gani tunaweza kutumia haya mawasiliano kwa tija, kujijenga na kujikwamua katika maswala mbali mbali. Kufahamu kuwa kutoelewa jinsi ya kuzitumia njia hizi, kuna sababisha madhara makubwa sawia na faida zitokanazo na kufahamu matumizi bora za mawasiliano haya.
Tukijifunza na kuheshimu mipaka na mazingira ya mawasiliano yetu, tutajenga jamii bora, yenye kupanua mawazo, kufurahisha, kustawisha mawasiliano na matokeo yake kuendelea kuwa bora kila siku.